Manqoba aichambua Gaborone United, atabiri mechi ngumu

Shabiki NambaMoja By Shabiki NambaMoja
β€’
4 Sep 2026
Manqoba aichambua Gaborone United, atabiri mechi ngumu

Kocha Mkuu wa Yanga, Manqoba Mngqithi, ametahadharisha kuwa mchezo dhidi ya Gaborone United hautakuwa mwepesi, akieleza kuwa wapinzani wao wana ubora mkubwa na wamejipanga vizuri katika maeneo mbalimbali ya uwanja.

Yanga inatarajiwa kushuka dimbani kesho Jumamosi katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, utakaopigwa katika Uwanja wa Taifa wa Botswana.

Akizungumza na wanahabari kuelekea mchezo huo, Mngqithi amesema kikosi chake kiko tayari kwa changamoto hiyo, huku akisisitiza umuhimu wa kucheza kwa umakini na kuepuka makosa ambayo yanaweza kuwapa Gaborone United faida wakiwa nyumbani.

Kocha huyo raia wa Afrika Kusini amesema amekuwa akifuatilia kwa karibu mwenendo wa Gaborone United na amevutiwa na kazi inayofanywa na kocha wao, Sean Connor.

“Tunakwenda kucheza mchezo ambao kwa kweli ni mgumu. Kwanza, lazima nimpe heshima Kocha Sean Connor. Nafikiri amefanya kazi kubwa sana na timu hii. Tangu alipoanza kuifundisha nimekuwa nikifuatilia kinachoendelea na naamini ameibadilisha na kuwa timu nzuri sana.”

Gaborone United wana ulinzi imara

Kwa mujibu wa Mngqithi, moja ya silaha kubwa za Gaborone United ni uimara wao katika safu ya ulinzi.

Amesema timu hiyo hairuhusu mabao mengi na pia ina uwezo wa kutumia vyema mashambulizi ya kushtukiza pamoja na mipira iliyokufa, hali ambayo Yanga italazimika kuwa makini nayo.

“Kwa upande wa ulinzi ni timu imara. Hairuhusu mabao mengi na pia ni hatari sana inapofanya mashambulizi ya kushtukiza pamoja na mipira iliyokufa (set pieces).”

Mngqithi pia amezungumzia kutokuwepo kwa Mothusi Johnson na Mpho Kgwaswane, akisema bado hawezi kutabiri kwa uhakika athari za kutokuwepo kwao kutokana na umuhimu waliokuwa nao kwenye kikosi.

Hata hivyo, amesema Gaborone United bado wana wachezaji wenye uzoefu na uwezo wa kuleta madhara, akiwemo kipa mwenye uzoefu, washambuliaji wawili wazuri na kipa kutoka Namibia, pamoja na beki wa kulia mwenye uwezo mkubwa.

Manqoba: Safu yao ya ulinzi ina uzoefu

Kocha huyo pia amefichua kuwa amefanya uchambuzi wa kina wa namna Gaborone United wanavyopanga safu yao ya ulinzi.

Amesema wana mabeki watatu wenye uzoefu wanaofanya vizuri katika majukumu yao, huku pia akimtaja beki wa kulia raia wa Nigeria kuwa mchezaji aliyemfuatilia kwa karibu.

“Wana safu ya ulinzi yenye uzoefu ikiwa na mabeki watatu ambao wanafanya vizuri sana katika majukumu yao ya ulinzi. Pia wana mwingine mzuri raia wa Nigeria, anayecheza upande wa kulia ambaye nimemfuatilia kwa karibu.”

Mngqithi amemtaja pia Kgamanyane kama mmoja wa wachezaji muhimu wa Gaborone United, akieleza kuwa ana uwezo wa kucheza kama kiungo mshambuliaji namba 10.

Kwa ujumla, amesema timu hiyo ina mfumo mzuri wa uchezaji, huku wachezaji wao wanne wa mbele wakibadilishana nafasi na kufanya mashambulizi kuwa magumu kutabirika.

Yanga yatakiwa kuwa makini kwenye transitions

Changamoto nyingine ambayo Mngqithi ameiona ni uwezo wa Gaborone United kufanya madhara pale wanapopata nafasi ya kushambulia baada ya mpinzani kupoteza mpira.

Amesema Yanga italazimika kuwa makini hasa katika kipindi cha mpito kutoka kwenye ulinzi kwenda kwenye mashambulizi.

“Ni timu ambayo tunapaswa kuwa makini nayo hasa katika nyakati za mpito kutoka kwenye ulinzi kwenda kwenye mashambulizi. Tunapaswa kuhakikisha tunakuwa imara katika ulinzi na pia kuboresha namna tunavyofanya counter pressing.”

Kocha huyo anaamini Yanga inaweza kupata matokeo mazuri ikiwa itatekeleza mpango wake wa mchezo kwa usahihi na kudhibiti maeneo ambayo Gaborone United wanaweza kupata nafasi za kushambulia.

Lengo ni kutawala mchezo

Licha ya kuonyesha heshima kubwa kwa Gaborone United, Mngqithi amesema Yanga haiendi Botswana kwa ajili ya kujilinda pekee, bali inalenga kutawala mchezo, kumiliki mpira na kujaribu kuhakikisha matokeo yanaamuliwa na namna wao watakavyocheza.

“Sisi ni timu itakayojaribu kutawala mchezo, kumiliki mpira na kuhakikisha kwamba matokeo ya mchezo yanaamuliwa zaidi na namna tunavyocheza na vitendo vyetu ndani ya uwanja.”

ADVERTISE HERE

Yanga SC Stories

Kundi la Yanga kama msimu uliopita tu
Kundi la Yanga kama msimu uliopita tu
7h ago
READ MORE β†’
Yanga yatupwa kundi B CAFCL
Yanga yatupwa kundi B CAFCL
7h ago
READ MORE β†’
Mzize ndio ameanza msimu hivyo
Mzize ndio ameanza msimu hivyo
11h ago
READ MORE β†’
Timu zinazoweza kukutana na Yanga makundi CAFCL
Timu zinazoweza kukutana na Yanga makundi CAFCL
12h ago
READ MORE β†’
Dladla alia na umaliziaji Yanga licha ya ushindi dhidi ya Mashujaa FC
Dladla alia na umaliziaji Yanga licha ya ushindi dhidi ya Mashujaa FC
16h ago
READ MORE β†’
Highlights: Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
Highlights: Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
16h ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumatano, Oktoba 28 2026
Magazeti ya leo Jumatano, Oktoba 28 2026
16h ago
READ MORE β†’
FT : Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
FT : Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
1d ago
READ MORE β†’
Magoli; Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
Magoli; Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
1d ago
READ MORE β†’
Kikosi : Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
Kikosi : Yanga vs Mashujaa Fc, NBC PL, Oct 27
1d ago
READ MORE β†’