Kocha Mkuu wa Yanga SC, Manqoba Mngqithi, ameweka wazi mpango wake wa kuhakikisha kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki anarejea kwenye ubora wake ili kuwa sehemu muhimu ya kikosi katika kampeni ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Yanga SC kesho Jumamosi inaanza rasmi kampeni yake ya michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa mchezo dhidi ya Gaborone United ya Botswana, utakaoanza saa 2:00 usiku kwa saa za Afrika Mashariki kwenye Uwanja wa Taifa wa Botswana.
Baada ya kukosekana kwenye mechi nne za mwanzo za ligi, Aziz Ki alirejea uwanjani katika mchezo dhidi ya Fountain Gate, ambapo alionesha umuhimu wake kwa kutoa pasi ya bao la kwanza lililofungwa na mshambuliaji Peter Shalulile.
Aziz Ki alicheza kwa muda mrefu katika mchezo huo kabla ya kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na Mudathir Yahya. Mudathir ndiye aliyeongeza bao la pili na kuiwezesha Yanga kupata ushindi wa 2-0.
Manqoba: Tunamhitaji Aziz Ki Ligi ya Mabingwa
Akizungumza baada ya mchezo huo, Manqoba alifichua kuwa Aziz Ki bado hajafikia asilimia 100 ya utimamu wake, lakini benchi la ufundi linafanya kila linalowezekana kumrudisha katika kiwango chake mapema.
“Aziz Ki ni mchezaji muhimu sana kwetu na tunamuhitaji kwenye mechi zijazo kwenye Ligi ya Mabingwa. Bado hayuko fit kwa asilimia 100 lakini tunampush ili kuhakikisha anakuwa tayari mapema,” alisema Manqoba.
Kauli hiyo inaonesha wazi kwamba Yanga inamuhitaji Aziz Ki kama sehemu ya mipango yake ya kufanya vizuri kwenye mashindano ya klabu yenye ushindani mkubwa zaidi barani Afrika.
Afanya mazoezi ya ziada
Katika kuhakikisha mpango huo unafanikiwa, Aziz Ki ameonekana akifanya mazoezi ya ziada baada ya kukamilika kwa programu za kawaida za mazoezi ya timu.
Hatua hiyo inaonesha ari na morali aliyonayo nyota huyo wa kimataifa wa Burkina Faso katika kuhakikisha anarejea kwenye kiwango bora na kuwa msaada mkubwa kwa Yanga katika msimu huu.
Kwa uwezo wake wa kutengeneza nafasi, kutoa pasi za mwisho na kufunga mabao, Aziz Ki anaweza kuwa miongoni mwa wachezaji muhimu katika safari ya Yanga kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wananchi wailenga fainali
Yanga imefanya usajili mkubwa huku sehemu kubwa ya mipango ya klabu ikiwa ni kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wananchi wameweka wazi dhamira yao ya kwenda mbali zaidi katika mashindano hayo, huku lengo likiwa ni kufika fainali.
Katika safari hiyo, utayari wa wachezaji muhimu kama Aziz Ki unaweza kuwa na nafasi kubwa. Ikiwa ataweza kufikia kiwango chake cha juu kwa wakati, Aziz Ki anaweza kuwa moja ya karata muhimu za Yanga katika harakati za kuandika historia mpya barani Afrika.