Mara baada ya mchezo uliopita wa ligi kuu dhidi ya JKT Tanzania, Kocha Mkuu wa Yanga Manqoba Mngqithi hakusita kutoa tathmini yake kuhusu kiwango cha kijana Juma Abushiri, maarufu kama Chuga Boy.
Manqoba alieleza kuwa hakuvutiwa sana na kile alichokiona kutoka kwa Chuga Boy katika mchezo huo, huku akimpa ushauri wa mambo ambayo alipaswa kuyafanyia kazi ili kuendelea kuboresha kiwango chake.
Kauli hiyo imekuja wakati ambapo Chuga Boy (18) ambaye alisajiliwa na Yanga kwenye dirisha lililopita akitokea klabu ya Fountain Gate, bado anaendelea kujenga uzoefu akiwa miongoni mwa vijana wanaopewa nafasi ya kuonyesha uwezo wao.
Hata hivyo, jana katika mkutano na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa leo dhidi ya Fountain Gate FC, Chuga Boy aliulizwa namna alivyoyapokea maoni ya Kocha Manqoba.
Kijana huyo hakutaka kutumia kauli za kocha kama sababu ya kukata tamaa, badala yake alizitazama kama sehemu ya safari yake ya kujifunza na kujijenga zaidi.
Akizungumzia hilo, Chuga Boy alisema:
“Cha kwanza nilichukulia positive ili inijenge. Bado mimi ni kijana mdogo, bado nina muda mwingi wa kujifunza. Kwahiyo ningechukulia negative, isingenijenga. Hata hivyo nilipata nafasi kwenye mchezo wa pili na nikaonesha,” alisema Chuga
Chuga Boy leo anaweza kupata nafasi ya kuwakabili waajiri wake wa zamani Fountain Gate katika mchezo utakaopigwa saa 10 jioni kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha.