Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, amesema marehemu Francis Kifukwe alikuwa miongoni mwa watu waliomsaidia kwa kiasi kikubwa katika safari yake ya uongozi ndani ya klabu hiyo, akieleza kuwa marehemu alimwelekeza mambo mengi na kumsaidia katika mchakato wa mabadiliko ya Yanga.
Hersi alitoa kauli hiyo leo katika Viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam wakati akitoa salamu za rambirambi kwa niaba ya Klabu ya Yanga wakati wa kumuaga Mwenyekiti wa zamani wa klabu hiyo, marehemu Francis Kifukwe, aliyefariki dunia hivi karibuni nchini India alipokuwa akipatiwa matibabu.
Hersi alimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwawezesha kufika katika siku hiyo, huku akiishukuru familia ya marehemu kwa kuruhusu Yanga kuandaa ibada maalumu ya kumuaga Kifukwe.
“Awali ya yote, nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia kufika katika siku hii. Nawashukuru sana wanafamilia kwa kuruhusu Klabu ya Yanga kuandaa ibada maalumu ya kumuaga Mzee Kifukwe,” alisema Hersi.
Alisema familia ilikuwa na ratiba na majukumu yake, lakini iliamua kuipa Yanga nafasi ya kumuaga kiongozi huyo wa zamani wa klabu.
“Tunafahamu kuwa wanafamilia walikuwa na ratiba zao na majukumu mbalimbali, lakini kwa upekee wao wameturuhusu sisi kama Klabu ya Yanga kupata nafasi ya kumuaga mpendwa wetu. Tunawashukuru sana kwa heshima hii kubwa,” alisema.
Hersi amshukuru Mangungu
Katika salamu zake, Hersi pia aliwashukuru wadau mbalimbali wa michezo waliojitokeza katika hafla hiyo, akimtaja kwa namna ya pekee Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu.
Hersi alisema uwepo wa Mangungu licha ya ushindani uliopo kati ya Yanga na Simba ni ishara ya heshima na mshikamano ndani ya familia ya soka.
“Niwashukuru wadau wote wa michezo ambao wamejitokeza siku ya leo. Kwa upekee, nimshukuru sana kaka yetu Murtaza Mangungu, Mwenyekiti wa Simba. Licha ya ugumu wa ratiba, amekubali kuungana nasi katika siku hii muhimu ya kumuaga Mzee Kifukwe,” alisema.
“Nimpongeze sana kwa ungwana wake na kwa kuonesha kwamba, pamoja na ushindani wetu wa kimichezo, bado tunaheshimiana na kuthaminiana kama familia ya soka.”
“Kifukwe alikuwa Injinia kama mimi”
Hersi alisema moja ya mambo yaliyomfanya ajihisi kuwa karibu na Kifukwe ni taaluma yao ya uhandisi, huku akimtaja marehemu kama mtaalamu aliyekuwa na mchango mkubwa katika masuala ya usajili na ujenzi wa timu.
“Kifukwe alikuwa Injinia kama mimi. Mzee Kifukwe anakumbukwa sana kwa utaalamu wake kwenye masuala ya usajili. Wapo watu ambao wamekuwa wakinifananisha na Mzee Kifukwe”
“Hata Pascal Kabombe huniuliza, ‘Kuna uhusiano gani kati ya u-Injinia na usajili?’ Lakini kama ilivyokuwa kwake, nasi tumekutana na majukumu haya ya kusajili wachezaji na kujenga timu,” alisema.
“Amenielekeza mambo mengi katika uongozi”
Hersi alisema uhusiano wake na Kifukwe ulikuwa wa karibu na kwamba marehemu alimsaidia katika mambo mbalimbali wakati wa uongozi wake ndani ya Yanga.
“Nimekuwa karibu sana na Mzee Kifukwe. Amenielekeza mambo mengi katika uongozi wangu na amenisaidia sana kwenye mchakato wa mabadiliko ya klabu,” alisema.
Alisema Kifukwe pia alitoa mchango katika kuhuisha kumbukumbu na nyaraka muhimu zilizokuwa na umuhimu katika safari ya mabadiliko ya Yanga.
“Amenisaidia kuhuisha baadhi ya kumbukumbu na nyaraka muhimu ambazo zilikuwa na mchango mkubwa katika safari hii,” alisema Hersi.
Hersi alifichua kuwa katika kipindi cha nyuma Yanga ilikuwa na makundi mbalimbali, ikiwemo Yanga Kampuni na Yanga Asili, hali iliyokuwa sehemu ya historia ya muundo wa klabu hiyo.
Hersi amebainisha kuwa Kifukwe alitoa mchango muhimu katika kusaidia kukamilisha mchakato wa mabadiliko ya klabu na kuunganisha historia hiyo na mfumo wa Yanga wa sasa.
“Hapo awali kulikuwa na makundi mengi ndani ya Yanga, kama Yanga Kampuni na Yanga Asili. Mzee Kifukwe ametusaidia kwenye kukamilisha mchakato wa mabadiliko, mchango wake kwangu na kwa Klabu ya Yanga ulikuwa mkubwa sana,” alisema.
Rais huyo wa Yanga amesema kifo cha Kifukwe siyo tu pigo kwa familia yake, bali pia ni pigo kwa Yanga na soka la Tanzania kwa ujumla kutokana na mchango alioutoa katika uongozi na maendeleo ya mchezo huo.