Kiungo Morice Chukwu raia wa Nigeria hayumo kwenye kikosi cha Singida BS kinachojiandaa na michuano ya CECAFA Kagame Cup nchini Rwanda.
Ni baada ya kiungo huyo kugomea mkataba mpya wa kuendelea kuwatumikia matajiri hao wa mkoani Singida.
Taarifa kutoka ndani ya uongozi wa Yanga imethibitisha kuwa tayari mabingwa hao wa soka Tanzania Bara 'wamepita' na kiungo huyo kiraka ambaye pia anamuda kucheza nafasi ya beki wa kati.
Ni suala la muda tu, Chukwu atatambulishwa kama mchezaji wa Yanga na kuanza maisha mapya na Wananchi ambao wameanza maandalizi yao Avic Town.
Chukwu anatua Yanga kuchukua nafasi ya Mohamed Damaro ambaye Yanga imesitisha mpango wa kumsajili moja kwa moja baada ya mkataba wa mkopo wa miezi sita kumalizika.
Damaro amerejea kwa waajiri wake Singida BS baada ya mpango huo wa kutua Yanga kukwama.