Klabu ya Yanga imeendelea kujiimarisha katika dirisha hili la usajili wakitajwa kuinasa saini ya kiungo mshambuliaji na winga machachari wa KMC FC, Eric Mwijage Edson.
Mwijage (24) ambaye alikuwa mmoja wa wachezaji tegemeo kwenye kikosi cha KMC kilichoshuka daraja msimu uliopita, amemwaga wino kuitumikia miamba hiyo ya Jangwani huku akitarajiwa kuongeza nguvu kwenye safu ya ushambuliaji ya Wananchi kuelekea mashindano ya ndani na yale ya kimataifa.
Awali, nyota huyo ambaye aliwahi kuitumikia Kagera Sugar, alikuwa akihusishwa na vilabu kadhaa vikiwemo Singida Black Stars na Pamba Jiji FC.
Sifa kuu ya Mwijage ni uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi za mbele (versatility), akimudu vyema kusimama kama winga wa pembeni au kiungo mchezeshaji wa nyuma ya mshambuliaji (attacking midfielder).
Yanga inafanya maboresho makubwa ya kikosi kwenye dirisha hili, Meneja wa Habari na Mawasiliano wa mabingwa hao wa nchi Ali Kamwe akidokeza kuwa yamefanyika maboresho makubwa yenye lengo la kukisuka upya kikosi ili kuhakikisha wanaendelea kutawala soka la ndani na kufanya vyema zaidi Kimataifa.