Wakati taarifa za ndani zikithibtisha kuwa klabu ya Yanga imemtoa kwa mkopo mshambuliaji Emmanuel Mwanengo, tayari mbadala wake amepatikana.
Mabingwa hao wa soka Tanzania Bara wanatajwa kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa Mashujaa Fc, Hussein Juma Mihambo.
Taarifa kutoka duru za usajili zimebainisha kuwa Yanga imekamilisha mchakato wa kumsajili mshambuliaji huyo chipukizi mwenye umri wa miaka 19.
Mihambo anatua kuongeza nguvu safu ya ushambuliaji akiwa ni mchezaji wa ndani.
Yanga imehitaji maboresho katika eneo hilo kwani mbali na Mwanengo kutolewa kwa mkopo, mshambuliaji mwingine Clement Mzize ni majeruhi na huenda akarejea kikosini mwezi Disemba.
Yanga imelazimika kurudi sokoni kuongeza nguvu katika mkakati wa maboresho ya kikosi kuelekea msimu mpya 2026/27.