Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema wachezaji Dickson Job na Clement Mzize wanaendelea na program maalum ya 'recovery' kabla ya kurejea kwenye majukumu yao kuwatumikia mabingwa hao wa kihistoria.
Kamwe amesema taarifa ya kitabibu kuhusu maendeleo ya nyota hao imebainisha kuwa watakuwa nje kwa wiki 10 au zaidi.
"Job na Mzize wanaendelea na program maalum, taarifa ya daktari imebainisha kuwa tunaweza kuwaona tena uwanjani mwishoni mwa mwezi wa Novemba au mwanzoni mwa Disemba," alisema Kamwe.
Kuhusu Pacome Zouzoua, Kamwe amesema nyota huyo raia wa Ivory Coast tayari ametoka hospitalini akitarajiwa kusafiri kuelekea Ufaransa kwa ajili ya matibabu zaidi.
Kamwe amesema mpaka sasa bado Pacome yuko chini ya uangalizi na taarifa zaidi kuhusu muda ambao atakuwa nje zinaweza kutolewa baada ya kipindi cha wiki sita za uangalizi kukamilika.
Ni wazi Pacome atakuwa nje kwa muda mrefu na Yanga inalazimika kuingia sokoni kusajili mbadala wake.