Klabu ya Geita Gold inatajwa kufungua mazungumzo na uongozi wa Yanga wakimuhitaji winga Edmund John kwa mkopo, imefahamika.
Mabingwa hao wa ligi ya Champonship ambao msimu ujao watashiriki ligi kuu ya NBC, wanahitaji huduma ya kiungo huyo mshambuliaji ambaye misimu michache nyuma aliwahi kuwatumikia kwa mafanikio kabla hawajashuka daraja na yeye kutimkia Singida BS.
Msimu uliomalizika Edmund alikuwa na vipindi tofauti kwenye kikosi cha Yanga changamoto ya jeraha la bega ikimuweka nje kwa muda mrefu.
Ni wazi bado ni mchezaji anayeweza kuwa na nafasi katika kikosi cha mabingwa hao wa nchi kwa kuzingatia mchango wake hasa katika mechi za kuelekea mwishoni mwa msimu uliopita.
Aidha katikaa hatua nyingine, klabu ya Singida BS nayo inatajwa kumuhitaji kiungo mshambuliaji Shekhan Khamis kwa mkopo.
Kama ilivyo kwa Edmund, Shekhan amekuwa na vipindi tofauti kwenye kikosi cha Yanga. Ushindani wa namba unamfanya asionekane mara kwa mara kikosini.