Msimu mpya wa Ligi Kuu NBC 2026/27 unatarajiwa kuanza rasmi katikati ya mwezi Agosti, huku kalenda ya soka la Tanzania ikibadilishwa kutokana na maandalizi ya michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 ambayo itaandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Kenya na Uganda.
Hizi ndizo tarehe muhimu ambazo mashabiki wa soka wanapaswa kuziweka alama kwenye kalenda zao:
Julai 6, 2026: Dirisha la usajili lafunguliwa
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilifungua rasmi dirisha kubwa la usajili tarehe Julai 6, likizipa klabu nafasi ya kusajili na kuimarisha vikosi vyao kuelekea msimu mpya.
Agosti 12, 2026: Yanga na Simba kuvaana Ngao ya Jamii
Mchezo wa Ngao ya Jamii utachezwa Agosti 12 na utawakutanisha mabingwa wa Ligi Kuu NBC, Young Africans (Yanga), dhidi ya mabingwa wa Kombe la CRDB Federation Cup, Simba SC.
Tofauti na misimu iliyopita, safari hii Ngao ya Jamii itahusisha mabingwa wa mashindano husika pekee, badala ya mfumo uliokuwa ukihusisha vilabu zaidi. Mabadiliko hayo yanalenga kupunguza msongamano wa ratiba kutokana na maandalizi ya AFCON 2027.
Agosti 14, 2026: Pazia la Ligi Kuu NBC lafunguliwa
Mashabiki wa soka nchini watashuhudia pazia la msimu wa 2026/27 likifunguliwa rasmi Agosti 14, huku timu zikianza mbio za kuwania ubingwa, nafasi za kushiriki michuano ya kimataifa na kupambana dhidi ya kushuka daraja.
Agosti 15, 2026: Dirisha kubwa la usajili lafungwa
Siku moja baada ya kuanza kwa ligi, dirisha kubwa la usajili litafungwa rasmi, ikiwa ni fursa ya mwisho kwa klabu kukamilisha usajili wa wachezaji kabla ya kusubiri dirisha dogo la usajili.
Mei 16, 2027: Msimu wa Ligi Kuu wafikia tamati
Ligi Kuu NBC inatarajiwa kumalizika Mei 16, 2027, takribani mwezi mmoja kabla ya kuanza kwa AFCON 2027. Ratiba hiyo imeandaliwa ili kutoa muda wa kutosha kwa maandalizi ya timu za taifa na shughuli nyingine zinazohusiana na michuano hiyo.
AFCON 2027 yaibadili kalenda ya soka
AFCON 2027 itaanza Juni 19 hadi Julai 17, 2027 nchini Tanzania, Kenya na Uganda. Kutokana na umuhimu wa mashindano hayo, TFF imelazimika kupanga ratiba ya ligi mapema zaidi ili kuhakikisha msimu unamalizika kwa wakati.