Rais wa Yanga, Injinia Hersi Said, amesema moja ya ahadi kubwa iliyosalia kwa uongozi wake ni kuhakikisha ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo katika eneo la Twiga na Jangwani, jijini Dar es Salaam, unaanza na kukamilika.
Hersi alitoa kauli hiyo leo, Julai 4, 2026, wakati wa sherehe za kuadhimisha ubingwa wa Ligi Kuu Bara, ambao Yanga imeutwaa kwa mara ya tano mfululizo.
Akizungumza katika makao makuu ya klabu hiyo, Jangwani, Hersi alisema mashabiki na wanachama wameendelea kumkumbusha ahadi ya kujenga uwanja wa kisasa, na kwamba uongozi umejipanga kuhakikisha mradi huo unaingia katika hatua ya utekelezaji.
“Paredi la msimu ujao tutakalofanya tutatafuta sehemu nyingine na si hapa tena Jangwani, kwa sababu mwakani ujenzi wa uwanja utakuwa unaendelea katika kipindi hicho,” alisema Hersi.
Alieleza kuwa hatua muhimu iliyobaki ni kukamilisha mchakato wa kubadili mfumo wa umiliki wa ardhi waliyopewa na Serikali kutoka umiliki wa wanachama kwenda kwenye kampuni maalumu itakayosimamia utekelezaji wa mradi huo.
Kwa mujibu wa Hersi, mabadiliko hayo yataiwezesha klabu kuendesha kwa ufanisi shughuli za uwekezaji na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa uwanja, ambao umekuwa miongoni mwa miradi mikubwa inayosubiriwa kwa hamu na wanachama na mashabiki wa Yanga.
Akizungumzia kuhusu mipango ya maboresho ya kikosi, Hersi alisema msimu huu walipata changamoto kidogo kutokana na baadhi ya wachezaji waliosajiliwa kushindwa kung'ra.
Hata hivyo katika dirisha hili watafanya usajili mkubwa ili kuhakikisha msimu ujao wanarejea wakiwa imara zaidi na kurejesha mataji yote waliyopoteza.
Nae mfadhili wa Yanga GSM amesema Yanga itaendelea kutwaa ubingwa 'Yanga Bingwa, mwakani tena..' alisema GSM alipopiga simu kuzungumza na mamia ya mashabiki waliojitokeza kwenye paredi la ubingwa Jangwani.