Mshambuliaji wa kimataifa wa Zimbabwe, Prince Dube, amejiunga rasmi na klabu ya Hardrock FC ya nchini Zimbabwe baada ya kumalizika kwa mkataba wake na mabingwa wa Tanzania Bara, Yanga SC.
Chanzo kutoka Zimbabwe kimethibitisha kuwa Dube amesaini mkataba wa miaka miwili utakaomuweka Hardrock FC hadi mwaka 2028, akianza rasmi sura mpya ya maisha yake ya soka baada ya kuitumikia Yanga kwa mafanikio makubwa kwa misimu miwili.
Uhamisho huo unamrejesha nyota huyo nchini kwao Zimbabwe, ambapo atakuwa sehemu ya kikosi cha Hardrock FC, moja ya klabu zinazokua kwa kasi katika soka la Zimbabwe. Klabu hiyo yenye makao yake Kwekwe ilipanda daraja hadi Ligi Kuu ya Zimbabwe baada ya kutwaa ubingwa wa Central Region mwaka 2025 na sasa inatumia Uwanja wa Chahwanda wenye uwezo wa kubeba mashabiki 15,000.
Dube anaondoka Yanga akiwa ameacha alama kubwa ndani ya kikosi hicho. Alijiunga na Wananchi mwaka 2024 akitokea Azam FC na akawa mmoja wa wachezaji waliochangia mafanikio ya klabu hiyo.
Katika msimu wa 2025/26, mshambuliaji huyo alifunga mabao 10 huku akiwa miongoni mwa wachezaji muhimu walioisaidia Yanga kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa msimu wa tano mfululizo. Mbali na mabao yake, Dube alionyesha uwezo wa kucheza nafasi mbalimbali za ushambuliaji, akitumika kama mshambuliaji wa kati na pia akitokea pembeni, jambo lililomfanya kuwa silaha muhimu katika kikosi cha Yanga.
Kiwango chake kizuri pia kimeendelea kuonekana akiwa na timu ya taifa ya Zimbabwe, ambapo amekuwa mmoja wa washambuliaji wanaotegemewa na Warriors katika mashindano ya kimataifa.
Kwa upande wa Hardrock FC, usajili wa Dube unaonekana kuwa sehemu ya mkakati wa kuijenga timu yenye ushindani mkubwa baada ya kupanda Ligi Kuu ya Zimbabwe. Klabu hiyo imekuwa ikiwekeza katika miundombinu na kikosi chake, ikiwemo kutumia Uwanja mpya wa Chahwanda, unaotarajiwa kuwa miongoni mwa viwanja vya kisasa nchini Zimbabwe.