Ilikuwa ni miezi, wiki, siku na sasa zimebaki saa chache kuelekea mchezo wa mwisho ligi kuu ya NBC msimu huu.
Yanga ina dakika 90 muhimu ugenini kuzisaka alama tatu katika mchezo dhidi ya JKT Tanzania.
Ni Okello Day, mechi hii ya ubingwa amekabidhiwa Star Boy Allain Okello akitarajiwa kuwaongoza wachezaji wenzake kusaka ushindi muhimu ambao utawahakikishia Wananchi ubingwa wa 32.
Ni wazi haitakuwa mechi nyepesi, sababu ni mechi inayoweza kuamua ubingwa, matumaini ya Simba kuwa bingwa pia yameshikiliwa na mchezo huo.
Ili kukata mzizi wa fitna, Yanga inahitaji ushindi kwani matokeo hayo yatatosha kuwapa ubingwa bila ya kujali wapinzani wao Simba watafunga mabao mangapi kwenye mchezo dhidi ya KMC.
Uwanja wa Isamuhyo leo unatarajiwa kupambwa kwa rangi za njano na kijani mashabiki wa Yanga wakitarajiwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia historia nyingine ikiandikwa.