Tetesi zimeendelea kushika kasi kuhusu klabu ya Yanga kuhusishwa na aliyekuwa kocha wa Raja Casablanca, Fadlu Davids, kuhusu uwezekano wa kuchukua nafasi ya ukocha mkuu wa mabingwa hao wa kihistoria.
Taarifa zinaeleza kuwa mabosi wa Yanga wamefungua rasmi mazungumzo na Fadlu ambaye msimu ulioipita aliinoa klabu ya Simba. Kocha huyo amepata bahati ya kufanya kazi katika klabu mbalimbali zenye ushindani mkubwa, huku akijijengea sifa ya kuunda timu zenye nidhamu ya kiufundi na uwezo wa kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa.
Hapa Tanzania alifahamika zaidi msimu uliopita akiongoza benchi la ufundi la Simba SC, ambapo alitoa mchango mkubwa katika kuijenga timu hiyo iliyofanikiwa kucheza fainali ya kombe la Shirikisho (CAFCC).
Fadlu aliachana na Raja Casablanca hivi karibuni kwa makubaliano ya pande mbili baada ya matokeo yasiyoridhisha, kufuatia kupoteza michezo miwili mfululizo katika Ligi Kuu ya Morocco, jambo lililopunguza matumaini ya klabu hiyo kutwaa ubingwa wa msimu huu.
Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, Yanga imekuwa ikimfuatilia kocha huyo kwa muda mrefu, ikiamini kuwa falsafa yake ya soka inaweza kuiwezesha timu hiyo kuendelea kutawala soka la ndani na kuongeza ushindani katika michuano ya CAF.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa mazungumzo hayo bado yako katika hatua za awali na hakuna makubaliano rasmi yaliyofikiwa. Pande zote zinaendelea kujadiliana kuhusu masharti mbalimbali kabla ya uamuzi wa mwisho kufanyika.
Iwapo dili hilo litakamilika, litakuwa miongoni mwa hatua zitakazovuta hisia kubwa katika historia ya soka la Tanzania. Kwa utamaduni wa ushindani uliopo kati ya Yanga na Simba, si jambo la kawaida kwa kocha mmoja kuzifundisha klabu hizo mbili, hata kama ni katika vipindi tofauti.
Historia inaonyesha kuwa ni makocha wachache sana waliowahi kupata nafasi hiyo. Marehemu Syllersaid Mziray anakumbukwa kama mmoja wa makocha wazawa waliowahi kuzinoa timu zote mbili. Kwa upande wa viongozi, hali hiyo pia ni nadra, huku Senzo Mbartha akiwa miongoni mwa waliowahi kuzitumikia Simba na Yanga katika nafasi ya Mtendaji Mkuu.
Uongozi wa Yanga umeweka wazi msimamo wake kuwa kwa sasa wameweka nguvu katika kuhakikisha wanatetea taji la ligi kuu kwa msimu wa tano mfululizo kesho wakitarajiwa kuhitimisha kwa mchezo dhidi ya JKT Tanzania ambao ushindi au pengine matokeo ya sare yanaweza kutosha Yanga kutetea ubingwa.
Baada ya msimu kumalizika, uongozi wa Yanga unatarajiwa kutangaza maamuzi kuhusu benchi la ufundi kuelekea msimu ujao. Makocha Abdihamid Moalin na Patrick Mabedi wanafanya vyema, licha ya kuwa tangu wakabidhiwe mikoba wamepoteza mechi mbili.