Kiungo mshambuliaji wa Yanga Allan Okello jana aliendelea kuthibitisha thamani yake akifunga hat-trik katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya TRA United na kuiweka Yanga kwenye nafasi nzuri ya kutetea taji la ligi kuu kwa msimu wa tano mfululizo.
Yanga imefikisha alama 72 na kimahesabu inahitaji angalau alama moja tu kurejesha ubingwa wa ligi kuu pale Jangwani.
Wananchi watahitimisha msimu kwa mchezo dhidi ya JKT Tanzania ambao utapigwa Jumanne, Juni 30 uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo.
Okello aliyetua Yanga mwezi Januari kwenye usajili wa dirisha dogo akitokea klabu ya Vipers Fc ya Uganda, amekuwa nguzo muhimu ya mafanikio ya kikosi cha Yanga.
Huyu ni mchezaji ambaye amejiunga na Yanga msimu ukiwa tayari unakaribia kufika nusu lakini mpaka sasa amezidiwa bao moja tu Feisal Salum 'Fei Toto' anayeongoza mbio za ufungaji bora akiwa na mabao 15 huku Okello akifikisha mabao 14 jana.
Mpaka sasa Yanga imefunga mabao 68, kati ya mabao hayo, Okello amehusika katika mabao 21 akifunga 14 na asisti 7.
Ukiwa umesalia mchezo mmoja tu, Okello ana nafasi ya kufanya maajabu pengine kuibuka mfungaji bora na kuingia kwenye kinyan'ganyiro cha tuzo ya MVP