Baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Azam Fc katika mchezo uliopigwa jana kwenye uwanja wa New Amaan Complex, Yanga sasa inaelekeza nguvu katika mchezo wa mzunguuko wa 29 dhidi ya TRA United.
Ni mtanange utakaopigwa Jumamosi, Juni 27 katika uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es salaam.
Wananchi wanahitaji kushinda mchezo huu ili kuukaribia ubingwa wa tano mfululizo katika ligi kuu ya NBC.
Lakini pia siku hii Yanga inaweza kutwaa ubingwa mapema endapo ikitokea watani zao Simba watakosa ushindi dhidi ya Singida Black Stars.
Baada ya Yanga kuwa kwenye presha kubwa kuelekea mchezo dhidi ya Azam Fc, pengine sasa watani zao Simba nao wanakwenda kukabiliana na presha ileile dhidi ya Singida BS.
Kwa Yanga ni kama ng'ombe ameshaliwa kilichobaki ni mkia tu kwani kimahesabu wanahitaji alama nne tu kutoka mechi mbili zilizobaki ili kuwa mabingwa.
Yanga itaingia kwenye mchezo wa Jumamosi ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa suluhu ya bila kufungana kwenye mchezo wa duru ya kwanza, hivyo watahitaji ushindi kwa gharama yoyote.
