Baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Azam Fc jana kwenye mchezo wa ligi kuu ya NBC, Yanga imefikisha alama 69 ambazo zimetosha kuwahakikishia tiketi ya kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika msimu ujao.
Katika mechi mbili zilizobaki ni Simba pekee iliyo nafasi ya pili ambayo inaweza kufikia alama ilizokusanya Yanga.
Matumaini ya Azam Fc kushiriki michuano hiyo yalikufa jana baada ya kipigo hicho kwani sasa wanaweza kufikisha alama 64 pekee.
Kwa maana nyingine ni kuwa Yanga na Simba tayari zimekata tiketi ya ligi ya mabingwa huku Azam Fc na Singida BS zikikata tiketi ya kushiriki kombe la Shirikisho msimu ujao.
Kazi iliyobaki kwa Wananchi sasa ni kuhakikisha wanatetea taji la ligi kuu kwa msimu wa tano mfululizo.
Jumamosi Yanga itakuwa uwanja wa KMC Complex kuikabili TRA United kabla ya kuhitimisha msimu kwa mchezo dhidi ya JKT Tanzania uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo siku ya Jumanne.