Klabu ya Yanga imepiga hatua kubwa katika harakati za kumrejesha kiungo mshambuliaji Stephane Aziz Ki kutoka klabu ya Al Ittihad ya Libya, imefahamika.
Aziz Ki yuko nchini kwa ajili ya mapumziko baada ya kukamilika kwa msimu mashindano nchini Libya.
Inaelezwa tayari Yanga imetuma ofa rasmi Al Ittihad kwa ajili ya kumsajili MVP huyo wa ligi kuu ya NBC msimu wa 2023/24.
Aziz Ki alitua Al Ittihad mwezi Januari kwenye dirisha dogo akijiunga na timu hiyo akitokea klabu ya Wydad CA ya Morocco.
Hata hivyo mwamba huyo kutoka Burkina Faso amepata hofu ya mazingira ya kiusalama huku pia akitaka kuwa karibu na familia yake.
Wakati Yanga ikiwa tayari imewasilisha ofa rasmi ya kumsajili, kama Al Ittihad hawatafikia makubaliano ya Yanga, huenda akafungua kesi FIFA kuishitaki klabu hiyo kwa kutokamilisha sehemu ya malipo yake ya fedha za usajili.
Kwa hali ilivyo, ni wazi Aziz Ki hayuko tayari kurejea Libya hivyo Yanga ina nafasi kubwa ya kumrejesha Jangwani.