Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe amesema kama mabingwa watetezi wa michuano ya kombe la CRDB wako tayari kulitetea taji hili.
Akizungumza katika mkutano wa matawi ya Wanayanga jijini Mwanza, Kamwe amewataka mashabiki na wanachama kujitokeza kwa wingi uwanja wa CCM Kirumba hapo kesho kwenye mchezo wa nusu fainali ya michuano hiyo dhidi ya Azam Fc utakaopigwa uwanja wa CCM Kirumba.
Kamwe amesema Azam Fc ni timu inayowapa ushindani kila wanapokutana hivyo wanatarajia mchezo mgumu.
Hata hivyo amesema kama mabingwa watetezi, watakwenda kupambana kwenye mchezo huo ili kuhakikisha wanatinga fainali ili kuweza kutetea taji la CRDB kwa msimu wa tano mfululizo.
“Tunatarajia mchezo mgumu na wenye ushindani mkubwa dhidi ya Azam FC hapa Mwanza. Napenda kuwahakikishia kuwa uongozi wa Klabu uko tayari, benchi la ufundi liko tayari, na wachezaji wetu pia wako tayari kwa ajili ya mechi hii muhimu."
"Sasa tunawaomba ninyi mashabiki wetu muonyeshe utayari wenu kwa kujitokeza kwa wingi uwanjani na kuipa timu sapoti inayostahili. Mwanza imekuwa ikitajwa kama ngome imara ya Yanga, na huu ndiyo wakati wa kuthibitisha hilo kwa vitendo."
"Tushirikiane katika maandalizi ya mchezo huu na tufike kwa wingi uwanjani ili kuwapa nguvu, hamasa na morali wapambanaji wetu wanapoingia uwanjani kutetea heshima ya Klabu yetu,” alisema Kamwe
Kamwe amebainisha kuwa ugumu wa mchezo dhidi ya Azam Fc pia unachangiwa na uimara wa benchi lao la ufundi linaloongozwa na kocha mwenye uzoefu mkubwa wa soka la Afrika, Florent Ibenge.
Amesema Yanga itawaheshimu Azam FC kwaa ubora wao lakini wanakwenda kwenye mchezo huo wakiwa na imani kubwa ya kushinda kutokana na maandalizi na ubora wa kikosi chao.
“Azam FC ni timu nzuri yenye ushindani mkubwa. Wana kocha mwenye uzoefu mkubwa katika michezo ya kiwango cha juu pamoja na wachezaji wenye ubora na uzoefu wa kutosha. Hata hivyo, kesho watakuwa wanakutana na YANGA."
"Klabu kubwa yenye historia, ubora na uzoefu mkubwa katika soka la Tanzania. Tunawaheshimu wapinzani wetu kwa kiwango chao, lakini tuna imani kubwa na maandalizi tuliyoyafanya, mshikamano uliopo ndani ya Klabu, ushirikiano mzuri wa matawi yetu pamoja na utayari wa wachezaji wetu. Kwa pamoja, tunaamini tutapambana kwa nguvu zote ili kupata ushindi utakaotuwezesha kutinga Fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB.”
“Kombe la Shirikisho la CRDB kwa sasa lipo mikononi mwetu kama mabingwa watetezi. Dhamira yetu sote ni kuona YANGA inalitetea taji hili na kutwaa ubingwa kwa mara ya tano mfululizo. Hata hivyo, azma hiyo haitafikiwa kwa urahisi bila sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wetu."
"Ndiyo maana nawasisitiza kujitokeza kwa wingi uwanjani kesho ili kuwapa nguvu na hamasa wachezaji wetu. Ratiba ya mashindano imekuwa ngumu na yenye msongamano mkubwa, huku kila mchezo uliobaki ukiwa na umuhimu wa kipekee. Katika kipindi hiki, wachezaji wetu wanahitaji sana sapoti yetu, na sauti zetu kutoka majukwaani zina mchango mkubwa katika kuwapa morali ya kuendelea kupambana kwa nguvu zote."
"Kesho ni siku muhimu kwa familia ya Wananchi. Amka mapema, jiandae vizuri, vaa kwa nadhifu na uje na familia yako, marafiki au mpenzi wako. Tukutane kwa wingi Uwanja wa CCM Kirumba kuisapoti na kuipambania YANGA yetu. Kwa pamoja, tuonyeshe nguvu ya Wananchi na tuwe sehemu ya safari ya kuelekea kutetea ubingwa wetu,” aliongeza Kamwe