Mlinda lango wa Yanga Aboutwalib Mshery amesema licha ya ugumu wa ratiba, wamejipanga kuhakikisha wanaibuka na ushindi kwenye mchezo wa nusu fainali kombe la CRDB dhidi ya Azam Fc.
Kesho Jumapili Yanga itaumana na Azam Fc kuisaka tiketi ya fainali ya kombe la CRDB mchezo utakaopigwa uwanja wa CCM Kirumba mkoani Mwanza.
Mshery amesema wachezaji wote wako tayari kwa mchezo huo muhimu, wanakwenda kupambana ili kuhakikisha wanapata ushindi na kutinga fainali.
"Ni kweli ratiba imekuwa sio rafiki sana mechi ziko karibu karibu lakini sisi tumejiandaa vyema kuelekea mchezo huo."
"Tunajua umuhimu wa mchezo huu, nia yetu ni kutetea ubingwa wetu hivyo tunahitaji kushinda ili tuingie fainali"
"Mchezo wa kesho ni mchezo wa kujitoa, tunaenda kukutana na wapinzani wazuri na wanaotaka pia kwenda fainali. Na sisi kama wachezaji tumejipanga kupambana na tunawaomba mashabiki wetu wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti," alisema Mshery
Yanga na Azam Fc zina siku tatu ngumu za maamuzi kwani baada ya mchezo huo, siku tatu baadae watarudiana tena kwenye mchezo wa ligi kuu ambao utapigwa Juni 24 uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.