Kocha Mkuu wa Yanga Abdihamid Moalin amesema maandalizi kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Fountain Gate utakaopigwa kesho Alhamisi kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mkoani Arusha yanakwenda vizuri.
Akizungumza kwenye mkutano na wanahabari kuelekea mchezo huo, Moalin amesema kikosi chake kiko tayari kukabiliana na Fountain Gate kwa namna yeyote ile watakayokuja nayo.
Moalin amesema anatambua haitakuwa mechi rahisi lakini ana imani na kikosi chake na watakwenda kupambana ili kuhakikisha wanapata ushindi.
"Tumekuwa na mwendelezo mzuri katika mechi tatu zilizopita, tumetengeneza nafasi nyingi na baadhi kuweza kuzitumia vyema. Lakini pia tumeonyesha uimara mkubwa katika ulinzi hatujaruhusu mipira mingi ya adhabu na kona, hii ni dalili nzuri kuwa tunawadhibiti wapinzani wetu katika maeneo sahihi."
"Tumecheza na timu zenye mbinu tofauti, nyingine zinajilinda kutokea nyuma wakisubiri mashambulizi huku nyingine zikijilinda kuanzia mbele 'high pressing' sisi tuko tayari kwa namna yoyote ambayo Fountain Gate watakuja"
"Naamini tuna wachezaji bora kwenye timu yetu ambao wanaweza kutusaidia katika mazingira yote," alisema Moalin