Mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara kwa misimu minne mfululizo, Yanga, wanatajwa kuonyesha nia ya kumsajili beki wa kati wa TRA United FC, Nassri Kombo, kuelekea dirisha kubwa la usajili la msimu ujao.
Kombo mwenye umri wa miaka 23 amekuwa miongoni mwa wachezaji waliovutia msimu huu kutokana na kiwango chake kizuri akiwa na TRA United. Uwezo wake wa kucheza kwa utulivu, kusoma mchezo na uimara wake katika safu ya ulinzi vimemfanya kuwa miongoni mwa mabeki wanaofuatiliwa kwa karibu na klabu kadhaa, huku Yanga ikionekana kuwa mbele katika mbio za kupata saini yake.
Taarifa zinaeleza kuwa Yanga imepanga kuongeza beki wa kati mzawa katika kikosi chake ili kuendelea kuimarisha ushindani wa ndani ya timu. Hatua hiyo inakuja wakati klabu hiyo ikitafuta mbadala wa Frank Assink, ambaye kwa sasa anaitumikia Yanga kwa mkopo akitokea Singida Black Stars.
Usajili wa Kombo unaweza kuipa Yanga nafasi ya kuendelea kuwa na msingi imara wa mabeki wazawa, huku ikielekeza nguvu zaidi katika kusajili wachezaji wa kigeni kwenye maeneo mengine muhimu, hususan safu ya kiungo na ushambuliaji.
Kwa sasa, Yanga haina presha kubwa katika eneo la ulinzi wa kati kutokana na uwepo wa mabeki wenye uzoefu kama Ibrahim Bacca, Bakari Mwamnyeto na Dickson Job, ambaye anatarajiwa kurejea kikosini wakati wa maandalizi ya msimu mpya 'pre-season'.
Mkataba wa Kombo na TRA United unatarajiwa kufikia tamati mwishoni mwa msimu huu, jambo linalomfanya kuwa mmoja wa wachezaji wanaoweza kupatikana kwa urahisi katika soko la usajili.