Wakati mashabiki wa Yanga wakisubiri kumalizika kwa msimu huu, mabosi wa klabu hiyo tayari wameanza mipango ya kukisuka upya kikosi chao kuelekea msimu ujao.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kuwa viongozi wa mabingwa hao wa Tanzania wameanza michakato ya awali ya usajili huku wakilenga kufanya maboresho makubwa katika kikosi kitakachoshiriki mashindano ya ndani na kimataifa msimu ujao.
Baada ya kutofanya vizuri katika dirisha kubwa la usajili lililopita, safari hii Yanga inataka kwenda kwa umakini zaidi ili kuhakikisha kila nafasi inayohitaji kuongezewa nguvu inapata mchezaji sahihi.
Chanzo kutoka ndani ya uongozi wa klabu hiyo kimeeleza kuwa Yanga inatarajia kufanya mabadiliko makubwa kwa wachezaji wa kigeni, ambapo nyota wasiopungua saba wanatajwa kuwa kwenye mipango ya kutua Jangwani mara dirisha litakapofunguliwa rasmi.
Iwapo mpango huo utakamilika, itamaanisha kuwa kati ya wachezaji 12 wa kigeni waliopo kwa sasa ndani ya kikosi hicho, ni watano pekee watakaobaki kuwa sehemu ya kikosi cha msimu ujao huku wengine wakiondoka kwa sababu mbalimbali ikiwemo kumalizana mikataba yao au kutokuwa kwenye mipango ya benchi la ufundi.
Tayari Yanga imeanza kusafisha kikosi chake kwa kuachana na baadhi ya wachezaji waliokuwa wametolewa kwa mkopo katika timu mbalimbali. Taarifa zinaeleza kuwa kiungo Mohamed Doumbia, Celestin Ecua, Jonathan Ikangalombo pamoja na Moussa Balla Conte hawatakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga msimu ujao baada ya klabu hiyo kuamua kutondelea nao.
Hatua hiyo ni sehemu ya mpango mpana wa maboresho unaolenga kutoa nafasi kwa wachezaji wapya watakaosajiliwa katika dirisha lijalo. Uongozi wa klabu unaamini kuwa mabadiliko hayo yatasaidia kuongeza ushindani ndani ya kikosi na kuimarisha maeneo ambayo yanaonekana kuhitaji maboresho katika msimu huu.
Mbali na wachezaji hao waliokuwa kwa mkopo, Yanga pia inatarajiwa kufanya tathmini ya mwisho kwa baadhi ya nyota waliopo kikosini kwa sasa. Wale ambao hawataonekana kuwa sehemu ya mipango ya benchi la ufundi kuelekea msimu ujao wataachwa ili kupisha usajili mpya.
Mabingwa hao wa Tanzania wanaonekana kuwa na malengo makubwa msimu ujao, si tu katika kutetea mataji ya ndani bali pia kufanya vizuri zaidi katika michuano ya kimataifa. Hali hiyo ndiyo inayowafanya viongozi wa klabu kuongeza umakini katika kila hatua ya usajili watakayoifanya.