Msemaji wa Yanga Ali Kamwe amesema kikosi kimerejea mazoezini wakijipanga kikamilifu kukabiliana na ratiba ya mechi mfululizo katika kipindi cha wiki mbili.
Katika muda wa siku 17 Yanga inatarajiwa kucheza mechi 6, tano zikiwa za ligi kuu na moja ikiwa ya nusu fainali kombe la CRDB. Ratiba hiyo inazikabili timu zote kwani Juni 30 msimu unapaswa kufika mwisho.
Kamwe amesema wamejipanga kutetea taji la ligi kuu kwa msimu wa tano mfululizo hivyo wanapaswa kuwa tayari kucheza katika mazingira yoyote yatakayowakabili.
"Ratiba ni ngumu lakini ukweli ni kwamba kila mtu ataonya machungu ya ratiba hii. Ukiangalia tuna mechi mbili za kusafiri mkoani lakini tumekubaliana na uhalisia."
"Kombe la Dunia linaanza wiki ijayo na ligi inapaswa kumalizika Juni 30 hivyo hakuna kulalamika wala kuweka visingizio," alisema Kamwe.
Yanga ilirejea KMC Complex jana kujiandaa na mchaka mchaka wa mechi mfululizo utakaoanza Juni 13 mkoani Kigoma kuikabili Mashujaa FC.
Baada ya mchezo huo Yanga itaelekea mkoani Arusha kuikabili Fountain Gate Juni 17 kisha kurejea jijini Dar es salaam kuikabili Azam Fc Juni 21 na Juni 24 mechi za nusu fainali kombe la CRDB na ligi.
Juni 27 Yanga itacheza dhidi ya TRA United dimba la KMC Complex na kisha kumalizana na JKT Tanzania Juni 30 uwanja wa Isamuhyo.