Timu ya taifa ya Zimbabwe imefanikiwa kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye michuano ya Unity Cup baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya India katika mchezo wa kutafuta mshindi wa tatu uliochezwa jijini London, Uingereza.
Shujaa wa Zimbabwe katika mchezo huo alikuwa mshambuliaji wa klabu ya Young Africans SC, Prince Dube, aliyefunga bao pekee la ushindi kwa njia ya mkwaju wa penalti dakika ya 33 ya mchezo.
Penalti hiyo ilitolewa baada ya mchezaji wa India, Farukh Choudhary, kumchezea vibaya Washington Navaya ndani ya eneo la hatari, na Dube hakufanya makosa alipoweka mpira wavuni na kuipa Zimbabwe uongozi uliodumu hadi mwisho wa dakika 90.
Mchezo huo uliochezwa katika Uwanja wa The Valley mjini London ulikuwa wa ushindani mkubwa, lakini Zimbabwe walionekana kuwa bora zaidi hasa katika sehemu kubwa ya kipindi cha kwanza na waliunda nafasi nyingi za kufunga. India walijaribu kusawazisha kipindi cha pili lakini walishindwa kupenya safu ya ulinzi ya Zimbabwe.
Ushindi huo umeifanya Zimbabwe kumaliza michuano ya Unity Cup 2026 katika nafasi ya tatu, huku India wakimaliza nafasi ya nne baada ya kushindwa kufunga bao lolote katika mashindano hayo.