RAIS wa Yanga, Injinia Hersi Said, anaingia kwenye moja ya kipindi muhimu zaidi tangu aanze kuiongoza klabu hiyo. Dirisha kubwa la usajili litakalofunguliwa Julai mwaka huu linaweza kuwa sehemu ya kuamua namna Yanga itakavyokuwa msimu ujao.
Kwa misimu kadhaa iliyopita, Yanga imekuwa timu bora zaidi Tanzania kwa mafanikio ya ndani na hata kimataifa. Ubora wa kikosi, ushindani mkubwa ndani ya timu pamoja na usajili wenye tija vilikuwa sehemu ya mafanikio hayo.
Hata hivyo, dalili zinaonyesha wazi kuwa nguvu ya kikosi imeanza kupungua. Tofauti na misimu iliyopita ambapo Yanga ilikuwa na wachezaji wenye uwezo wa kubadilisha mchezo hata kutoka benchi, msimu huu kikosi kinaonekana kuwa finyu katika baadhi ya maeneo muhimu.
Moja ya sababu kubwa ni kushindwa kufanya usajili wenye tija katika madirisha mawili yaliyopita. Idadi kubwa ya nyota waliosajiliwa hawakuweza kuendana na kiwango cha ushindani wa Yanga, hali iliyosababisha baadhi yao kuondoka ndani ya muda mfupi.
Majina kama Ecua Celestin, Moussa Balla Conte, Mohamed Doumbia na Andy Boyeli yalikuja na matarajio makubwa, lakini mambo hayakwenda kama ilivyotarajiwa. Wengi wao walishindwa kujihakikishia nafasi ya kudumu kwenye kikosi cha kwanza na hatimaye wakaachwa baada ya miezi sita pekee.
Katika dirisha dogo, Yanga ikaongeza nguvu kwa kuwasajili nyota wengine kama Allan Okello, Buba Jammeh, Mohamed Damaro pamoja na Depu. Kati ya hao, Okello ameonekana kuendana haraka na mfumo wa timu huku akianza kuwa mhimili muhimu kikosini.
Damaro amekuwa akitumika kulingana na mahitaji ya mechi, wakati Depu alianza vizuri kabla ya majeraha kumrudisha nyuma na kupunguza kasi yake na kuonyesha ubora wake.
Kwa sasa ukweli unabaki kuwa Yanga inahitaji maboresho makubwa ikiwa inataka kuendelea kutawala soka la Tanzania na kufanya vizuri kimataifa. Ushindani wa ligi unaongezeka huku timu nyingine zikianza kuwekeza zaidi kwenye vikosi vyao.
Dirisha lijalo halihitaji tena majaribio mengi ya wachezaji wasiokuwa na uhakika. Yanga inahitaji usajili wa moja kwa moja wa wachezaji wenye uwezo wa kuingia kwenye kikosi cha kwanza na kuleta tofauti mapema.
Injinia Hersi na uongozi wake wana kazi kubwa ya kuhakikisha makosa yaliyopita hayajirudii. Mashabiki wa Yanga sasa wana matarajio ya usajili wenye ubora, ushindani na wenye kuendana na malengo makubwa ya klabu hiyo.
Iwapo maboresho sahihi hayatofanyika, basi msimu ujao unaweza kuwa mgumu zaidi kwa Yanga katika mashindano ya ndani na Kimataifa.