Jana lilitokea tukio la kushangaza baada ya benchi la ufundi la Singida BS kumfanyia mabadiliko mlinda lango Metacha Mnata dakika ya 15 baada ua kufungwa bao kupitia mpira wa adhabu uliopigwa na Allan Okello.
Ni tukio la kushangaza kwa sababu Metacha sio golikipa wa kwanza kufungwa bao kama lile, wanafungwa magolikipa bora huko duniani.
Okello alipiga mpira kiufundi na kumpoteza mlinda lango kwani hakutarajia kama mpira ule ungeweza kupitishwa kwenye eneo finyu ambao alikuwa amepanga ukuta.
Mijadala mingi inaibuliwa mitandaoni kimkakati, kuna watu walitamani kuona Yanga inapoteza dhidi ya Singida BS baada ya mambo kuwa tofauti wameamua kufanya propaganda.
Benchi la ufundi la Singida BS hawakumtendea haki Metacha kwani tukio lile la kumtoa baada ya kufungwa ni sawa na kumchafua wakati amefungwa kama sehemu ya mchezo.
Hata hivyo golikipa aliyeingia baada ya Metacha kutolewa mbona nae aliruhusu mabao mwili bao la tatu likikaribia kufanana na lile alilofungwa Metacha?
Nadhani kwa tukio lile alipaswa kusifiwa Okello kwa ufundi wake aliotumia kwenye kupiga mpira na sio kulaumu magolikipa.
Misimu michache nyuma Stephane Aziz Ki alikuwa na aina yake ya upigaji wa faulo ambao ulisumbua magolikipa wengi. Magolikipa waliingia kwenye lawama kama ilivyotokea kwa Metacha jana.
Bahati mbaya zaidi ni kuwa mambo haya huonekana yakifanywa na wachezaji wa Yanga lakini kwa timu nyingine hutayasikia.
Huu ni ujumbe kwa Wananchi kuwa kuna jitihada kubwa za 'kuwadogosha' na kuwafanya msiamini uwezo wa timu yenu kila mara inaposhinda.
Yanga inapofeli kuna watu wananufaika! Ndio maana kabla ya mchezo dhidi ya Dodoma Jiji walisema ni mechi kati ya Anthony na Mavunde lakini baada ya Yanga kupoteza walikesha wakishangilia.
Hivyo hata jana dhidi ya Singida BS walitamani yajitokeze yale ya Dodoma Jiji lakini haikuwezekana sasa wamebaki kwenye propaganda nyepesi.