Baada ya kukosekana kwenye mchezo wa robo fainali kombe la CRDB dhidi ya JKT Tanzania, nahodha wa Yanga Bakari Nondo Mwamnyeto amerejea kikosini kuendeleza mapambano ya kutetea mataji mawili yaliyobaki yaani ligi kuu na kombe la CRDB.
Mwamnyeto alipewa ruhusu maalum baada ya mchezo dhidi ya Dodoma Jiji ambao Yanga walipoteza kwa mabao 3-2.
Baada ya mashambulizi mengi mitandaoni pamoja na ukosoaji, nahodha mwenye makombe mengi zaidi kwenye historia ya Yanga amerejea kuongoza mapambano. Wanasema kila binadamu hupitia changamoto, ndivyo ilivyo kwa wachezaji kwani nao ni binadamu.
Ni wazi yale yaliyotokea katika mchezo dhidi ya Dodoma Jiji ilikuwa siku mbaya kazini kwake, na sasa amerejea kufanya kilichobora zaidi.
Mwamnyeto amekuwa beki tegemeo kwenye kikosi cha Yanga kwa takribani misimu mitano, makosa ya mechi moja hayawez kumuondolea heshima yake.
Habari njema pia ni kurejea kikosini kwa beki wa pembeni Israel Mwenda ambaye nae alikosekana kwenye mechi zilizopita kutokana na changamoto ya majeraha.
Mara ya mwisho Mwenda aliitumikia Yanga kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba uliopigwa uwanja wa Isamuhyo na kumalizika kwa matokeo ya sare ya mabao 2-2.