Mapema leo Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lilitangaza ratiba ya mechi za nusu fainali kombe la CRDB Yanga ikitarajiwa kuchuana na Azam Fc mchezo utakaopigwa Juni 21 uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Itakuwa ni wiki ya dabi ya Dar es salaam kwani baada ya mchezo huo, siku tatu baadae yaani Juni 24 Yanga na Azam Fc zitachuana tena katika mchezo wa ligi kuu ya NBC.
Kuna rekodi ya aina yake Yanga imeweka kwenye michuano ya kombe la CRDB, msimu huu Wananchi wakilisaka taji la tano mfululizo.
Yanga imecheza mechi 28 kwenye michuano hiyo bila kupoteza. Kwa lugha rahisi ni kuwa Yanga imeshinda mechi 28 mfululizo kwenye michuano hiyo inayoendeshwa kwa mfumo wa mtoano.
Endapo Yanga itatwaa taji hilo msimu huu, itaweka rekodi ya aina yake ambayo pengine itachukua muda mrefu kuvunjwa kwani Wananchi watakuwa wamecheza mechi 30 bila kupoteza sawa na kushinda kila mechi msimu mzima.
Licha ya ugumu wa ratiba iliyo mbele, Meneja wa habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema kila mechi wataikabili kwa kuzingatia uzito wake lengo likiwa kutetea mataji yote mawili yaani ligi kuu na CRDB.