Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema mfadhili wa klabu hiyo Ghalib Said Mohammed 'GSM' hana tamaa katika uwekezaji wa uwanja wa klabu hiyo.
Jana klabu ya Yanga ilisaini makubaliano ya ujenzi wa uwanja eneo la Jangwani ambao utachukua takribani mashabiki 20,000, GSM akichukua jukumu la kutoa fedha katika makubaliano ya 50-50 na Yanga ambayo imetoa eneo la kujenga uwanja huo.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Kamwe alimpongeza GSM kwa kujitoa kwake bila ya kuweka tamaa kwenye umiliki wa uwanja huo kwani angeweza kuhitaji asilimia 80 kwake na 20 kwa klabu hiyo.
"Unajua kuna wakati unaweza kuwa na tamaa lakini GSM ni tofauti sana hebu angalia anataka asilimia 50 tu lakini ingekuwa mwingine angehitaji hata asilimia 80 ziwe kwake na klabu tubaki na 20,"amesema Kamwe
"Sisi Yanga tunakushukuru kwa moyo wako unatupa somo kwamba tuache tamaa kwenye maisha yetu na nadhani GSM amekuwa hataki mambo mengi kuna ile kauli yake ya Yanga bingwa lakini sasa tumuongezee maneno haya; hana tamaa."
Baada ya makubaliano hayo kusainiwa jana, mchakato wa ujenzi umeanza rasmi leo ambapo baada ya kupata vibali, wakati wowote Wananchi watashuhudia kazi ikiendelea Jangwani.
Uwanja huo unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi 18 hadi 20 na kuzinduliwa rasmi tayari kutumika.