Mshambuliaji wa Yanga Prince Dube, ameendeleza kiwango bora baada ya kurejea kutoka majeraha, akionyesha makali makubwa katika safu ya ushambuliaji huku akiisaidia timu yake kupata matokeo chanya.
Takwimu zinaonesha kuwa Dube amefunga mabao sita katika michezo sita ya hivi karibuni aliyoichezea Yanga katika mashindano mbalimbali, kiwango kinachoashiria kurejea kwake kwa nguvu baada ya kukaa nje kwa muda.
Katika mfululizo huo wa mechi, mshambuliaji huyo alianza bila kufunga dhidi ya TMA Stars FC, kabla ya kufunga mabao mawili dhidi ya Mbeya City na kuendeleza ubora wake kwa kufunga mawili mengine dhidi ya Muembe Makumbi City katika Kombe la Muungano.
Aliendelea kuonesha mchango wake kwa kufunga bao moja dhidi ya Azam FC, kabla ya kukosa kufunga katika mchezo wa fainali ya Kombe la Muungano dhidi ya Simba SC. Hata hivyo, alirejea kwenye orodha ya wafungaji kwa kufunga bao moja katika mchezo wa Ligi Kuu NBC dhidi ya Simba SC.
Mbali na kiwango chake katika mechi hizo za hivi karibuni, Dube pia anaendelea kung’ara katika mbio za kuwania kiatu cha ufungaji bora wa Ligi Kuu NBC msimu huu. Kwa sasa, amefikisha mabao tisa, akilingana na kiungo mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum, ambao wote wanaongoza orodha ya wafungaji.
Dube amefanyia kazi baada ya changamoto zilizokuwa zinamkabili akiongeza ufanisi mbele ya lango, nidhamu ya hali ya juu pamoja na uwezo mzuri wa kutumia nafasi chache anazopata.
Ni wazi Dube ni mmoja wa wachezaji tegemeo katika kikosi cha Yanga ambao wanatizamwa kama wachezaji muhimu wa kuipa Yanga mafanikio msimu huu.