Mlinzi wa Yanga Mohamed Hussein 'Zimbwe Jr' amesema wachezaji wote wako tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba utakaopigwa kesho Jumapili kwenye uwanja wa Isamuhyo.
Zimbwe Jr amesema wanatambua umuhimu wa mchezo huo katika mkakati wa kutetea taji la ligi kuu kwa msimu wa tano mfululizo.
Licha ya kukiri uimara wa wapinzani wao Simba, Zimbwe Jr amesema Yanga pia ina kikosi bora na kesho watahakikisha wanaongeza ubora zaidi ili kushinda mchezo huo.
"Sisi wachezaji tumejiandaa vizuri na tunakwenda kumalizia maandalizi jioni ya leo, tuna imani tunakwenda kufanya vizuri hapo kesho kwakuwa kila mmoja wetu anatambua. Umuhimu wa alama tatu za kesho"
"Kila mmoja anatambua ubora wa wapinzani wetu, lakini pia tunatambua ubora wetu, kwenye mapungufu yetu tunakwenda kuyafanyia kazi na kwenye ubora tunakwenda kuongeza, tuna amini kuwa tunakwenda kukusanya alama tatu hapo kesho"
"Ukipoteza mchezo wa kesho maana yake kwenye mbio za ubingwa utakuwa una suasua, hivyo tunatambua umuhimu wa kushinda kesho ili tuongeze gap la alama kati yetu na mpinzani wetu," alisema Zimbwe Jr.