Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves amesema maandalizi ya kikosi chake kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Simba yanakwenda vizuri.
Goncalves amesema leo watakamilisha maandalizi hayo akiwaahidi mashabiki wa Yanga kuwa watarajie mchezo tofauti kutoka kwa timu yao siku ya Jumapili
"Tumekuwa na siku tatu za maandalizi kuelekea mchezo wa Jumapili. Huu ni mchezo wa ligi hivyo tumejiandaa na mpango tofauti."
"Leo tutakuwa na maandalizi ya mwisho ya kimkakati. Tunasikitika hatukupata matokeo mazuri kwenye mchezo uliopita lakini naamini tuko katika njia sahihi kuelekea mchezo unaofuata."
"Tuna matumaini na matarajio mkubwa ya kufanya vizuri hapo kesho, naamini mashabiki wetu watakuja kwa wingi uwanjani kutuunga mkono. Hii ni nafasi muhimu kwetu kuongeza gap la pointi juu ya msimamo kufikia alama nane dhidi ya wapinzani wetu," alisema Goncalves
Akizungumzia mchezo uliopita, Goncalves amesema licha ya kukosa ushindi kwenye mchezo huo, aliridhishwa na kiwango kilichoonyeshwa na wachezaji.
Amewahakikishia mashabiki wa Yanga kuwa timu yao iko tayari na itaingia na mbinu tofauti kwenye mchezo wa Jumapili ili kuchukua alama zote tatu.
Goncalves pia alieleza masikitiko yake kwa kumkosa kiungo Mudathir Yahya katika mchezo huo akifungiwa siku chache kabla ya mchezo.
Kocha huyo raia wa Ureno ameonesha kushangazwa na kufungiwa kwa Muda katika mazingira ambayo mchezo uliopita mshambuliaji wa Simba Suleiman Mwalimu hakuadhibiwa mpaka pale mchezo wa dabi ya Kariakoo ulipochezwa.
Hata hivyo Goncalves amesema haitakuwa mara ya kwanza kumkosa Muda, hivyo atatumia wachezaji wengine walio tayari kuchukua nafasi yake.