Kesho Jumapili, macho ya wapenda soka Tanzania yataelekezwa katika dimba la Meja Jenerali Isamuhyo ambapo dabi nyingine ya Kariakoo itapigwa, safari hii Yanga wakiwa wageni wa watani wao wa jadi, Simba, katika mwendelezo wa Ligi Kuu ya NBC.
Huu utakuwa mkutano wa pili wa timu hizi ndani ya siku tano pekee, kufuatia pambano la fainali ya Kombe la Muungano lililopigwa Aprili 29, ambapo Simba waliibuka na ushindi mwembamba wa bao 1-0.
Matokeo hayo yameongeza uzito wa dabi ya kesho, hasa kwa upande wa Yanga ambao wanaingia uwanjani wakiwa na dhamira mbili kuu: kurejesha heshima na kujikusanyia alama muhimu.
Kwa upande wa Wananchi, huu si mchezo wa kawaida. Mbali na hitaji la pointi tatu ili kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi, pia ni fursa ya kulipiza kisasi kufuatia kipigo cha Jumatano iliyopita.
Kwa misimu takribani mitatu mfululizo, Yanga walikuwa na rekodi nzuri dhidi ya Simba, wakionyesha ubabe wao kwenye mechi za dabi. Hata hivyo, ushindi wa Simba katika mchezo uliopita umeweka doa kwenye rekodi hiyo, jambo linalowapa Yanga hamasa ya kipekee ya kurejea kwa nguvu.
Ishara ya uzito wa mchezo huu ilionekana mapema, baada ya Yanga kurejea mazoezini haraka siku ya Alhamisi, siku moja tu baada ya kipigo hicho. Benchi la ufundi lilichukua hatua ya kipekee kwa kupendekeza kikosi kisalie visiwani Zanzibar kwa maandalizi maalum, wakilenga kuwajenga wachezaji kimwili na kisaikolojia kabla ya kurejea Bara kwa ajili ya pambano hilo.
Licha ya matokeo ya mchezo uliopita, Yanga bado wanajivunia rekodi bora katika ligi dhidi ya Simba, wakiwa hawajapoteza katika michezo mitano iliyopita ya ligi dhidi ya watani wao hao. Hii inawapa morali kubwa kuelekea mchezo wa kesho, wakilenga kuendeleza ubora huo na kuongeza pengo la pointi.
Kwa sasa, Yanga wanaongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 47 baada ya michezo 19, wakifuatiwa na Simba walio nafasi ya pili kwa tofauti ya pointi tano. Ushindi wa kesho utaifanya Yanga kufikisha tofauti ya pointi nane, faida kubwa katika mbio za ubingwa.