Mlinzi wa kushoto wa Yanga SC, Chadrack Boka, anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi kitakachoshuka dimbani leo dhidi ya Simba SC kwenye fainali ya Kombe la Muungano itakayopigwa katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Boka anarejea kikosini akiwa katika kiwango kizuri, baada ya kuanza kwenye mchezo wa nusu fainali ulioshuhudia Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Azam FC.
Katika fainali ya leo, beki huyo anachukua nafasi ya Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’, ambaye anakosekana kutokana na majeraha.
Jukumu kubwa linalomkabili Boka ni kuhakikisha anadhibiti mashambulizi ya Simba yanayotokea pembeni, hasa kupitia kwa mawinga wao Libasse Gueye na Anicet Oura.
Upande wa kushoto wa Yanga, anaocheza Boka, unatarajiwa kuwa moja ya maeneo yenye ushindani mkubwa kutokana na uwepo wa Gueye ambaye katika mchezo uliopita alimpa wakati mgumu Zimbwe Jr.
Hata hivyo, kasi ya Boka inaweza kwendana na winga huyo kutoka Senegal huku uwezo wake wa kupanda kushambulia ukitarajiwa kuipa Yanga faida.
Katika upande huo, kuna uwezekano pia wa Kocha Pedro Goncalves kumtumia Pacome Zouzoua kama winga, jambo ambalo linaweza kufungua zaidi nafasi kwa Boka kufanya mashambulizi ya kushtukiza, hasa iwapo Simba wataamua kuelekeza nguvu kubwa katika kumkaba Pacome.
Fainali ya leo inatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa, ni dakika 90 zitakazokuwa na thamani kubwa kwa kila mchezaji.