Hatimaye ile siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini imewadia. Ni mchezo wa fainali ya kombe la Muungano kati ya Yanga dhidi ya Simba utakaopigwa uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar.
Ni Kariakoo Derby, mchezo wa tatu kuzikutanisha Yanga na Simba tangu kuanza kwa msimu huu wa 2025/26.
Watani hao wa jadi walikutana Septemba 16 2025 kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii, Pacome Zouzoua akifunga bao pekee la Yanga lililowahakikishia Wananchi kutwaa Ngao.
March 1 2026 mchezo baina ya timu hizo wa ligi kuu ya NBC ukapigwa uwanja wa New Amaan Complex, matokeo yakiwa suluhu ya bila kufungana.
Sasa timu hizo zinakutana tena katika uwanja wa New Amaan Complex katika mchezo mwingine ambao lazima mshinda apatikane iwe ndani ya dakika 90 au mikwaju ya penalti.
Yanga ndio mabingwa watetezi wa kombe la Muungano wakilitwaa taji hilo baada ya kuifunga JKU kwenye mchezo wa fainali msimu uliopita.
Ni nafasi nyingine kwa Wananchi kuhakikisha taji hilo linarudi kabatini pale Jangwani kwa msimu wa pili mfululizo.
Hata hivyo haitakuwa mechi nyepesi mbele ya watani zao Simba ambao wamecheza mechi 7 mfululizo dhidi ya Yanga bila kupata ushindi.
Wakati huu Yanga inaelekea kwenye mchezo huo ikiwa kwenye kiwango bora zaidi kulinganisha na mara ya mwisho timu hizo zilipokutana March 01.
Uwepo wa kiungo mshambuliaji Pacome Zouazoua ni faida kubwa kwa Yanga akikosekana katika mchezo uliopita kutokana na jeraha la bega.
Pacome amefunga mabao mawili katika mechi mbili za mwisho alizocheza dhidi ya Simba, akiwa amefunga mabao matatu katika mechi zote.
Hivyo ni mchezaji ambaye aliamua matokeo ya dabi zilizopita na bila shaka leo tena anaweza kurudia kila alichofanya kwenye mechi hizo.
Kiufundi pia Yanga imebadilika, ujio wa Kocha Msaidizi Abdulhamid Moalin umeleta mabadiliko ya kuchezaji Wananchi sasa wakicheza soka la kushambulia kwa kasi tofauti na vile walivyoanza msimu.
Mashabiki wa Yanga leo wanatarajia kuiona timu yao ikishambulia zaidi kuliko vile ilivyocheza mechi iliyopita ambapo kwa muda mwingi walicheza kwa kujihami.
Kimsingi ni mchezo unaotarajiwa kuwa na mashambulizi kutoka kila upande, umakini wa safu ya ulinzi na matumizi ya nafasi ndio kitu pekee kitakachoamua matokeo ya mchezo huo.