Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe ametamba kuwa timu hiyo imejipanga kutetea taji la Muungano kwa msimu wa pili mfululizo, wakipania kushinda mchezo wa nusu fainali dhidi ya Azam Fc.
Juzi Yanga iliichapa Muembe Makumbi mabao 4-0 na kukata tiketi ya nusu fainali ambapo mabingwa hao watetezi wanakutana na Azam Fc katika Dar es salaam Derby.
"Sisi tumejipanga na dhamira yetu ni kutetea taji hili la Muungano kwa msimu wa pili mfululizo"
"Niwaambie Wananchi wanaopanga safari ya kuja Zanzibar, nawaomba bebeni hela ya kutosha kukaa huku mpaka fainali," alitamba Kamwe.
Kama Yanga itafanikiwa kuichapa Azam Fc katika mchezo wa nusu fainali utakaopigwa uwanja wa New Amaan Complex kesho Jumamosi, upo uwekano Derby ya Kariakoo ikapigwa mapema visiwani Zanzibar kama Simba nayo itashinda mchezo wa nusu fainali dhidi ya Mlandege Fc utakaopigwa Jumapili.
May 03 Simba na Yanga zitachuana kwenye mchezo wa ligi kuu katika Kariakoo Derby inayosubiriwa kwa hamu na mashabiki wa soka nchini.