Kiungo mshambuliaji wa Young Africans SC, Shekhan Khamis, ameanza kuonyesha dalili wazi za kukomaa kisoka na kuwa tayari kubeba majukumu makubwa ndani ya kikosi hicho kinachonolewa na Pedro Gonçalves.
Katika mwendelezo wa kiwango chake kizuri, Shekhan aliibuka shujaa juzi baada ya kuiongoza Yanga kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Muungano, akifunga bao moja katika ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Muembe Makumbi. Kiwango chake kilimfanya achaguliwe kuwa nyota wa mchezo huo, akionyesha ubora mkubwa katika eneo la kiungo na ushambuliaji.
Licha ya kutomaliza mchezo huo kutokana na majeraha madogo aliyoyapata, mchango wake uliweka wazi namna ambavyo anaendelea kuwa muhimu ndani ya kikosi cha mabingwa hao wa Tanzania Bara.
Akiwa katika msimu wake wa pili tangu ajiunge na Yanga, Shekhan ameanza kuonyesha mabadiliko makubwa ya kiuchezaji, akiongeza kujiamini, ubunifu na uwezo wa kuamua matokeo ya mechi. Hali hiyo imeongeza imani kwa benchi la ufundi.
Kocha Gonçalves ameendelea kumpa nafasi zaidi msimu huu, ishara kuwa anaamini katika uwezo wake na mchango anaoweza kutoa katika malengo ya timu hiyo, kutetea mataji yote ya ndani.
Ni suala la muda tu, Shekhan atakuwa mmoja wa wachezaji muhimu wanaoweza kuibeba Yanga.
