Beki tegemeo wa Young Africans SC Ibrahim Bacca, ameendelea kuwa gumzo ndani na nje ya Tanzania huku kiwango chake kikizidi kuvutia macho ya vigogo wa soka barani Afrika.
Taarifa za hivi karibuni zinaeleza kuwa klabu ya Raja Club Athletic (Raja CA) imerejea tena Jangwani kwa dhamira ya kutaka kuinasa saini ya beki huyo kisiki. Hii si mara ya kwanza kwa miamba hiyo ya Morocco kuonesha nia, jambo linaloashiria namna wanavyovutiwa na uwezo wake.
Katika dirisha dogo la usajili lililopita, Raja walifanikiwa kumsajili kiungo Moussa Balla Conte kwa mkopo, huku wakibakiza nafasi ya kumsajili moja kwa moja iwapo ataridhisha. Sasa macho yao yameelekezwa kwa Bacca, wakiamini anaweza kuimarisha zaidi safu yao ya ulinzi.
Inatajwa kuwa kocha wa Raja, Fadlu Davids, ambaye msimu uliopita aliinoa Simba SC, ndiye anayesukuma dili hilo. Akiwa anaifahamu vizuri soka ya Tanzania, Davids anaamini Bacca ana uwezo wa kufanya vizuri kwenye ligi ya Morocco na michuano ya kimataifa.
Pamoja na mvuto huo, bado Yanga haijaonyesha dalili za kuwa tayari kumuuza mchezaji huyo muhimu ambaye ana mkataba hadi mwaka 2027. Hata hivyo, kama ilivyo kawaida ya soka la kisasa, ofa kubwa inaweza kubadilisha msimamo wa klabu hiyo.
Bacca, aliyejiunga na Yanga Januari 2022 akitokea KMKM SC, ameendelea kukua na kuwa mhimili mkuu wa ulinzi wa mabingwa hao wa Tanzania Bara. Mbali na klabu, pia ni mchezaji wa timu ya taifa, Tanzania, ambapo ameonyesha kiwango cha juu kinachozidi kumtangaza kimataifa.
Jambo la kipekee kuhusu Bacca ni kwamba pia ni askari anayehudumu KMKM akiwa na cheo cha sajenti, huku akiwa amepewa ruhusa maalum ya kuitumikia Yanga.