Kocha Mkuu wa Yanga Pedro Goncalves amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mbeya City utakaopigwa kesho Alhamisi, April 16 katika uwanja wa KMC Complex.
Licha ya kutambua ugumu wa mchezo huo, Pedro amesema ana imani na kikosi chake na watakwenda kupambana ili kuhakikisha wanapata alama tatu.
Aidha amesema urejeo wa mshambuliaji Prince Dube aliyekuwa nje kutokana na majeraha unampa matumaini ya kufanya vizuri zaidi katika mchezo huo.
"Mchezo wa mwisho nillifanya mabadiliko kadhaa ili kutoa fursa kwa baadhi ya wachezaji kupata utimamu wa kimwili, ulikuwa wasaa mzuri pia kupumzisha baadhi ya nyota wetu. Hivyo nina matarajio hapo kesho kuwa ufanisi wa wachezaji wangu utakuwa mkubwa na malengo yetu ni kupata alama tatu pamoja na kutoa burudani kwa mashabiki wetu"
"Mechi ya mwisho ugenini dhidi ya Mbeya City ulikuwa mchezo mgumu sana kutokana na hali ya uwanja, kesho tutacheza kwenye mazingira tofauti ambayo tumeyazoea. Nakiri sisi tupo imara zaidi na tunauhitaji mkubwa wa alama tatu. Nafaham hata wao wanahitaji alama lakini kwetu ni hadithi nyingine, ninajiamini kwa kiwango kikubwa kuwa timu yangu ipo kwenye ufanisi mzuri sana wa kimbinu na kiufundi."
"Licha ya kwamba tunahitaji alama tatu kwa namna yoyote ile lakini tunapaswa kuwa na tahadhari. Lazima tuwaheshimu wapinzani wetu. Mbeya City wana kikosi kizuri chenye uzoefu mkubwa. Umakini ndio nguzo yetu kwa hapo kesho. Mpira ni mchezo wa makosa ukifanya kosa moja linaweza kugharimu mchezo mzima"
"Nina matarajio makubwa kwa kesho baada ya urejeo wa Prince Dube, mchezo uliopita alipata dakika 14 baada ya kutoka kwenye majeraha ujio wake utaongeza nguvu na ufanisi kwenye eneo la ushambuliaji. Bado Depu hajaanza kurejea uwanjani hivyo kurejea kwa Dube kutaleta matumaini makubwa kwetu. Tunaratajia kumkosa Mwanengo pia, lakini ni kazi yetu kama benchi la ufundi kutafuta njia mbadala ya kuziba pengo la majeraha," alisema Goncalves