Rais wa Klabu ya Yanga, Injinia Hersi Said, ameweka wazi msimamo wa klabu hiyo na kufunga mjadala unaoendelea kuhusu kiungo Mohamed Damaro, ambaye hivi karibuni amekuwa gumzo kubwa kwenye soka la Tanzania.
Sakata hilo lilichukua sura mpya baada ya Klabu ya Simba kuwasilisha malalamiko katika Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ikipinga usajili wa Damaro kama mchezaji wa ndani. Hata hivyo, TFF ilichunguza suala hilo na hatimaye kutupilia mbali madai hayo, ikisisitiza kuwa taratibu zote za usajili zilifuatwa kikamilifu kulingana na kanuni zilizopo.
Akizungumza katika mahojiano na TBC Online, Hersi alisema wazi kuwa Yanga haina uhusiano wowote na mjadala huo, kwani ilimsajili Damaro akiwa tayari ametambuliwa rasmi kama raia wa Tanzania.
“Yanga SC hatuhusiki na lolote kuhusu uraia wa Damaro. Tulimsajili akiwa tayari ameidhinishwa na Uhamiaji na kutangazwa rasmi kama mchezaji wa Kitanzania,” alisema Hersi.
Aidha, alieleza kuwa Damaro alipata uraia wa Tanzania mwaka 2025 wakati akiwa na klabu ya Singida Black Stars, kabla ya kujiunga na Yanga kwa mkopo.
Tangu wakati huo, mchezaji huyo ametambulika na mamlaka za soka nchini kama mchezaji wa ndani kwa mujibu wa sheria.
Katika hatua nyingine, Injinia Hersi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Vilabu Afrika (ACA), na Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya FIFA, ameteuliwa na Bodi ya Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) kuwa Balozi wa Kiswahili ndani na nje ya mipaka ya Tanzania.
Mhandisi Hersi atakuwa miongozi mwa mabalozi watatu wa BAKITA ambao ni Mama Salma Kikwete na Jorum Mkumbi