Mlinda lango Aboutwalib Mshery anatarajiwa kufanyiwa uchunguzi zaidi wa jeraha la goti alilopata wakati kikosi cha Yanga kikikamilisha maandalizi kuelekea mchezo wa ligi kuu dhidi ya Pamba Jiji uliopigwa uwanja wa CCM Kirumba juzi.
Mshery alikosa mchezo huo ambao Yanga iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 huku Hussein Masalanga akiliweka salama lango la mabingwa hao wa nchi.
“Mshery hakuonekana kwenye mchezo dhidi ya Pamba baada ya kuumia goti kwenye mazoezi yetu ya mwisho, ndiyo maana alidaka Masalanga."
“Wakati madaktari wakifuatilia maendeleo yake na atafanyiwa vipimo zaidi ili kujua ukubwa wa jeraha lake, kwa hiyo tutawajulisha majibu ya madaktari,” amesema bosi mmoja wa Yanga.
Yanga ilirejea Dar jana ambapo kesho Jumamosi itacheza mchezo wa Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya TMA ikiwa ni hatua ya 16 bora na Masalanga anatarajiwa kuendelea kukaa langoni.
Mlinda lango namba moja Djigui Diarra atakosa mchezo huo ukiwa wa tatu na kumaliza rasmi adhabu yake ya kufungiwa mechi tatu.
Diarra tayari amekosa michezo dhidi ya Tanzania Prisons na Pamba Jiji.