Baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tanzania Prisons katika mchezo uliopita wa ligi kuu ya NBC, kikosi cha Yanga sasa kinaelekea jijini Mwanza kwa ajili ya mchezo unaofuata dhidi ya Pamba Jiji.
Jumatano April 08 katika uwanja wa CCM Kirumba, Yanga watakuwa wageni wa Pamba Jiji katika mchezo mwingine unaotarajiwa kuwa na upinzani mkali.
Mabingwa hao watetezi wanahitaji kushinda mchezo huo ili kuendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi.
Baada ya watani zao Simba kutoka suluhu ya bila kufungana dhidi ya Azam Fc jana, matokeo hayo yameongeza wigo wa uongozi wa Yanga kuwa tofauti ya alama sita kileleni huku Yanga ikiwa imecheza mechi moja zaidi.
Hata ikitokea Simba wakashinda mechi yao ya kiporo dhidi ya TRA United, Wananchi bado wana uhakika wa kuendelea kusalia kileleni kwa tofauti ya alama tatu.
Ni wazi kwa sasa hakuna nafasi ya kudondosha tena alama kwa kocha Pedro Goncalves na vijana wake ili kuhakikisha mpango wa kutetea ubingwa kwa msimu wa tano mfululizo unafanikiwa.