Mshambuliaji hatari wa Yanga Laurindo Aurelio 'Depu' ameanza mazoezi ikiwa hatua muhimu kuelekea kurejea kikosini.
Depu alikuwa nje ya uwanja akiuguza majeraha ya misuli akiungana na nyota kadhaa wa Yanga ambao walikosekana kwenye mechi za mwishoni kabla ya mapumziko ya kalenda ya FIFA.
Kurejea kwa kinara huyo wa mabao kwenye kikosi cha Yanga ni habari njema kwa Wananchi kuwa sasa wanakwenda kuendeleza mapambano ya kutetea ubingwa wakiwa na kikosi kamili.
Kulikuwa na hofu kuwa Depu angekaa nje kwa muda zaidi kutokana aina ya jeraha alilopata lakini mshambuliaji huyo kutoka Angola amepambana kuhakikisha anarejea mapema.
Akiwa amejiunga na Yanga kwenye usajili wa dirisha dogo, Depu ana namba za kutisha kwani katika mechi 10 ameweka kambani mabao 11 kwenye michuano yote.
Kwenye ligi ya NBC amefunga mabao 6 sawa na mshambuliaji mwenzake Prince Dube ambaye pia tayari ameanza mazoezi ya Gym ukiwa ni mchakato kabla ya kurejea kikosini kikamilifu.




