Jana Rais wa Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Patrice Motsepe alikumbushia bao walilofunga Yanga kwenye mchezo dhidi ya Mamelodi wakati akitangaza mabadiliko na maboresho katika Katiba na Kanuni zake yatakayoongeza imani na uwazi kwa waamuzi, wasimamizi wa VAR pamoja na vyombo vya kimaamuzi vya shirikisho hilo.
Motsepe amewataja mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara katika hotuba yake wakati akitoa ufafanuzi wake huko Cairo, Misri katika mkutano maalumu na waandishi wa habari uliofanyika Misri
Tukio ambalo Motsepe aliligusia ni bao la Yanga ambalo lilikataliwa mwaka 2024 katika mechi ya robo fainali ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Mamelodi Sundowns na kufanya mechi hiyo kumalizika suluhu hivyo, Wananchi kutupwa nje kwa mikwaju ya penalti 3-2.
"Kama ulitazama kwenye TV wakati ule Yanga inacheza na Mamelodi lile lilikuwa ni bao halali na nimekuwa nikisema hivyo mara nyingi, kumekuwa na juhudi nyingi kuhakikisha tunatoka huko na ndicho hiki tunachofanya sasa," alisema na kuongeza.
“CAF kwa sasa inatekeleza mabadiliko makubwa katika Katiba na Kanuni zake ambayo yataongeza imani kwa waamuzi wa CAF, waendeshaji wa VAR, makamishna wa mechi pamoja na Bodi ya Nidhamu na Rufaa ya CAF. Maboresho haya pia yatahakikisha kuwa matukio yasiyokubalika yaliyojitokeza katika AFCON Morocco 2025 hayatatokea tena,” alisema rais huyo.
Stephane Aziz Ki alifunga bao hilo ambalo liliibua mjadala mkali kila pembe ya Afrika lakini mwisho wa siku Yanga ikawa imekosa nafasi ya kuandika historia kwa kucheza nusu fainali ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika.
