Kikosi cha Yanga siku ya Jumatatu, March 30 2026 kinatarajiwa kurejea mazoezini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons ambao utapigwa April 04 uwanja wa KMC Complex.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema timu itarejea mazoezini wakiwa na ari mpya baada ya mapumziko ya takribani wiki moja.
"March 30 timu itangia kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Tanzania Prisons ambao utapigwa kwenye uwanja wa KMC Complex."
"Wachezaji wote ambao hawana changamoto zozote za kiafya pamoja na benchi la ufundi ambalo limeongezewa nguvu na kocha Msaidizi Abduhamid Moalin, wako tayari kwa ajili ya kuimarisha Yanga ili iendeleze vipigo kwenye ligi," alisema Kamwe.
Kamwe pia amezungumzia hali ya wachezaji majeruhi ambapo amesema wachezaji wanne tayari wameanza mazoezi ya Gym na wanaweza kuungana na wenzao mazoezini siku ya Jumatatu.
Kamwe amewataja Prince Dube, Edmund John, Chadrack Boka na Ibrahim Bacca kuwa wanaendelea vizuri huku mshambuliaji Laurindo Aurelio 'Depu' akiwa bado kwenye uangalizi wa daktari pengine akihitaji wiki moja zaidi kabla ya kurejea kikosini.