Baada ya kikosi cha Yanga kurejea jijini Dar es salaam mapema leo wakitokea mkoani Dodoma ambako jana walikamilisha mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar, kutakuwa na takribani mapumziko ya kalenda ya FIFA, siku 10.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema katika kipindi cha mapumziko hayo, uongozi chini ya Rais Injinia Hersi Said wanatarajiwa kukutana kufanya tathmini ya mechi za mzunguuko wa kwanza.
Kamwe amesema licha ya kumaliza mechi za mzunguuko huo wakiwa kileleni mwa msimamo, tathmini inalenga kuangazia maeneo yote ikiwa ni pamoja na yale waliyofanya vyema ili wayaendeleze na yale ambayo hawakufanya vyema ili wafanye maboresho.
"Maoni yamekuwa mengi kutoka kwa Wanachama na Mashabiki wetu lakini niwaambie tuweni watulivu, viongozi wetu ni wasikivu na yale ya msingi yote naamini yatafanyiwa kazi," alisema Kamwe.
Kumekuwa na presha kubwa kutoka kwa baadhi ya wanachama na mashabiki ambao wanataka uongozi ufanye maboresho katika benchi la ufundi baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa timu katika mechi za hivi karibuni.
Katika mechi tano zilizopita kwenye ligi, Yanga imeshinda mechi mbili tu na kutoka sare tatu mtawalia dhidi ya Azam Fc, TRA United na Mtibwa Sugar.