Yanga imedondosha alama mbili mkoani Dodoma iikilazamishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Mtibwa Sugar.
Wananchi walizihitaji alama zote tatu leo ili kuanza vyema mzunguuko wa pili na walikaribia kuondoka nazo kama sio bao la dakika za lala salama lililofungwa na Mtibwa Sugar.
Ni mchezo ambao pia ulitawaliwa na matukio mengi, ikiwa ni pamoja na tukio la mlinda lango Djigui Diarra kuonekana amefanyiwa madhambi wakati akijaribu kuokoa kona iliyoinyima Yanga alama tatu.
Lakini pia kipindi cha kwanza kulikuwa na tukio la pasi ya Mudathir Yahya kwa Pacome Zouzoua kuamuliwa kuwa ni offside wakati alikuwa eneo sahihi.
Ni wazi waamuzi wa mchezo huo wanaweza kuadhibiwa kwa matukio hayo lakini matokeo hayawezi kubadilika.
Ligi inakwenda kusimama kwa takribani wiki mbili kupisha kalenda ya FIFA, bila shaka Yanga itarejea ikiwa imara zaidi baada ya mapumziko.
Baadhi ya wachezaji ambao ni majeruhi wakiwemo washambuliaji Prince Dube na Depu wanaweza kurejea kikosini baada ya mapumziko.
Njia ya uhakika kwa Yanga kushinda mechi hasa katika duru hii ya pili ni kuhakikisha wanatumia vyema nafasi na kufunga mabao mengi.
Leo Yanga ilikuwa na nafasi ya kufunga mabao zaidi ya moja lakini umakini ulikosekana eneo la umaliziaji.