Meneja wa Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Ali Kamwe amewataka Wanachama na Mashabiki wa timu hiyo kuepuka matukio ya kufanya vurugu viwanjani kwa matukio hayo yanapelekea adhabu kwa klabu kila mara.
Kamwe ametoa kauli hiyo baada ya Kamati ya saa 72 ya TFF kuipa Yanga faini ya Tsh Milioni 10 kutokana na matukio ya mashabiki yaliyojitokeza kwenye mechi zilizopita.
"Nimeona ni vyema leo kuzungumza na Wanachama pamoja na Mashabiki wetu. Jana jioni, kupitia taarifa ya Bodi ya Ligi, sote tulishuhudia adhabu ya faini iliyotolewa kufuatia vitendo vya baadhi ya Wanachama na Mashabiki wetu kurusha chupa uwanjani katika mchezo wetu wa ugenini dhidi ya Azam FC."
"Hii ni mara ya pili kwa Klabu yetu kutozwa faini ya aina hii. Ni muhimu kufahamu kuwa adhabu hizi zina athari kubwa kifedha na zikiendelea mwisho wake hautakuwa mzuri kwa maendeleo ya Klabu yetu."
"Napenda kuwaomba Wanachama na Mashabiki wetu wote kudumisha ustaarabu wanapofika uwanjani kuishangilia Klabu yetu. Furaha inapopatikana, tushangilie na pale ambapo kuna jambo halijaridhisha, tunaweza kuonesha hisia zetu kwa njia za amani kama vile kuzomea lakini si kwa kurusha chupa au vitu vingine hatarishi wala kusababisha fujo."
"Vitendo vya namna hiyo havina nafasi katika soka letu na si sehemu ya utamaduni tunaotaka kuujenga. Tushirikiane kulinda taswira ya Klabu yetu na kuhakikisha mazingira ya uwanjani yanabaki kuwa salama yenye heshima na yanayovutia kwa kila mmoja," alisema Kamwe.
Katika hatua nyingine, Kamwe amewapongeza mashabiki wanaosafiri kutoka mikoani kuelekea Dodoma kuipa sapoti Yanga kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Jamhuri.
Kamwe amesema hivi ndivyo mashabiki wanapaswa kufanya, kuiunga mkono timu katika nyakati zote.
"Nimefurahishwa sana na namna Wanachama na Mashabiki wetu walivyopokea matokeo ya michezo yetu iliyopita. Aidha, tayari magari zaidi ya 50 yameondoka jijini Dar es Salaam kuja hapa Dodoma kwa lengo la kuja kuiunga mkono Klabu yetu."
"Msimu uliopita, katika nyakati kama hiki tulipoteza dhidi ya Azam FC pamoja na Tabora. Hata hivyo, napenda kuwataarifu Wanachama na Mashabiki wetu kuwa nyakati ngumu zimepita na mabadiliko hayo mtayaona kuanzia mchezo wa kesho dhidi ya Mtibwa Sugar"