Meneja wa habari na Mawasiliano wa Yanga Ali Kamwe amesema Yanga ndio timu bora zaidi nchini kwa sasa na ndio maana wengine wanaitumia kama kipimo chao cha kuimarika
Kamwe amesisitiza kuwa wataendelea kupambana ili kuhakikisha wanatimiza malengo yao ya kutwaa ubingwa wa ligi kuu na kutetea mataji yote wanayoshikilia.
"Bado hakuna timu bora na iliyokamilika kama Yanga, kwa hiyo tunatambua daraja ambalo tuko nalo sisi ni kipimo cha timu zote nchini."
"Timu inayopata sare na Yanga inaamini imepanda uwezo kwani wapinzani wetu wanaamini si rahisi kupata ushindi mbele yetu."
"Sisi tunatambua daraja letu ni la kuchukua ubingwa ndio maana watu wanaotoa maoni sisi kama taasisi ambayo ina viongozi makini tunayachakua."
"Yaliyo maoni mazuri tunayafanyia kazi lakini yale mengine ambayo sio mazuri tunaachana nayo lengo likiwa kuboresha zaidi."
"Itakapofika mwishoni mwa msimu hakuna timu itakumbukwa kwa kupata sare na Yanga, itakumbukwa timu iliyotwaa ubingwa," alisema Kamwe.
Kamwe ametoa kauli hiyo akijibu hoja tofauti miongoni mwa wachambuzi, mashabiki na wadau wa soka juu kiwango kilichoonyeshwa na Yanga kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Azam Fc uliopigwa juzi Jumapili uwanja wa Benjamin Mkapa na kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana.